Gå direkte til innhold
Startsiden Om UNE UNE in other languages Hii ni Bodi ya Rufaa ya Uhamiaji (UNE)

Hii ni Bodi ya Rufaa ya Uhamiaji (UNE)

UNE ni chombo cha utawala kinachoweza kulinganishwa na mahakama, ambacho hushughulikia malalamiko au rufaa za kukataliwa maombi au madai fulani na Directorate of Immigration (UDI) (Idara ya Uhamiaji nchini), kufuatana na Sheria ya Uhamiaji na Sheria ya Uraia ya Norway. Kiutawala, UNE imewekwa chini ya Ministry of Justice and Public Security (Wizara ya Haki na Usalama). Ijapokuwa Wizara inasimamia utawala wa UNE kwa kupitia sheria, kanuni, bajeti na aula za kijumla, lakini haiwezi kutoa mwongozo juu ya ufafanuzi wa sheria, utambuzi na ufahamu wa maamuzi, au maamuzi katika kesi fulani.

Maombi ya rufaa yanayoshughulikwa na UNE ni yale yanayohusu kimbilio la hifadhi ya kisiasa, uhamiaji wa familia, vibali vya kuishi, kufukuzwa nchini na uraia.

UNE ina wafanyakazi zaidi ya mia tatu na hamsini, baina yao wakiwemo Viongozi 30 wenye elimu ya kimahakama. Pamoja na hao kuna wananchi 300 wasio weledi ambao wamejitolea na kujishughulisha kama wajumbe wa bodi.

UNE ina njia zaidi ya moja ya kukata shauri au kufikia maamuzi. Maamuzi yanaweza kutolewa kwenye mkutano wa bodi ya rufaa wakati mkata rufaa mwenyewe akiwa amehudhuria, hali kadhalika kwenye mkutano wa bodi bila mkata rufaa kuhudhuria, yanaweza kutolewa na mwenyekiti wa bodi baada ya kupitiwa na katibu wa kisheria au yanatolewa na katibu wa kisheria. Mwenyekiti mmoja huamua utaratibu wa kuendesha kila kesi ya rufaa.

Kufuatana na Sheria ya Uhamiaji (Immigration Act) kesi za rufaa zisizo na shaka huweza kufanyiwa maamuzi yake bila ya mkutano wa bodi ya rufaa, na hufanyiwa maamuzi hayo na mwenyekiti peke yake au na ofisi ya usimamizi na urasimu. Hizi huwa miongoni mwa kesi za rufaa zile ambazo zinaambatanika kwa urahisi kikanuni, ambapo huwa rahisi kuthibitisha kama matakwa au masharti maalumu katika sheria na kanuni yametimizwa. Ni hasa maombi ya rufaa yaliyokuwa na shaka dhahiri hupelekwa mbele ya bodi ya rufaa.

Mikutano mingi ya bodi ya rufaa huitishwa wakati mkata rufaa mwenyewe akihudhuria. Lakini vile vile mikutano mingine hutendeka bila mkata rufaa mwenyewe kuwepo. Kwa mfano ikiwa mkata rufaa na Idara ya Uhamiaji nchini wamekubaliana juu ya uhakika fulani wa kimsingi kuhusu kesi fulani ya rufaa, yaani maelezo ya mkata rufaa yametiwa maanani wakati kesi ilipowasilishwa UNE, basi mkutano wa bodi ya rufaa unaweza kuitishwa bila mkata rufaa kuhudhuria. Kwa upande mwingine kuhudhuria kwa mkata rufaa ni muhimu pale ambapo kuwepo kwake kunachangia katika kufafanua uhakika fulani katika kesi.

Kwenye mikutano ya bodi ya rufaa, hushiriki mwenyekiti mmoja wa bodi pamoja na wajumbe wawili wa bodi wasio weledi. Katibu wa kisheria wa UNE anatayarisha kesi ambazo zitashughulikiwa kwenye mkutano wa bodi ya rufaa. Mwenyekiti wa bodi ya rufaa huwasilisha nyaraka za daawa kwa wanachama watakaoshiriki kwenye mkutano kabla ya mkutano huo. Mikutano kama hii hufanywa kwa siri.

Mikutano ya bodi ya rufaa hufunguliwa kwa kutolewa muhtasari, waliopo wanatambulishwa na mkata rufaa anaulizwa maswali. Kesi za rufaa zinaposikilizwa, mkata rufaa atajibu maswali ya bodi na ya mwakilishi (mwanasheria) wao. Mwakilishi anapewa nafasi ya kutoa muhtasari wa kesi. Kesi za rufaa ambazo hushughulikiwa katika mikutano ya bodi ya rufaa maamuzi yake hutolewa kwa wingi wa kura.

Maamuzi yanayotolewa katika daawa mbalimbali, hayawezi kupitiwa upya na wizara, serikali au na uongozi wa UNE. Lakini rufaa inaweza kukatwa kwa kupitia mfumo wa kawaida wa kisheria.

Imepitiwa upya tarehe 13.11.12